Website za Wapendwa


Thursday, October 13, 2011

Jitambue Ya Chris Mauki.....SABABU MBOVU ZA KUINGIA KATIKA NDOA

Watu wengi tumewaona kwenye ndoa wakiishi katika hali tofauti za maisha, wako wenye fedha na wasionazo, wako wenye furaha na wasio na wasionao. Yote hii huweza kuchangiwa na sababu nyingi ikiwemo wanandoa hawa kujikuta wanaingia katika ndoa wakisukumwa na sababu zilizo mbovu na zisizo na msingi. 

Ziko sababu njema na nzuri za ndoa zinazoongelewa sana na wengi maeneo mbalimbali.  Mimi nimejaribu kuzitafuta zile sababu zisizo nzuri ambazo wengine pasipokuwa makini wamezishikilia na kusiruhusu sababu hizi ziwasindikize katika ndoa na hivyo kujikuta wenajuta na kulia katika muda mwingi wa maisha.

Hii pia ni sababu ya ukweli kwamba siku hizi idadi ya ndoa zinazovunjika ni kubwa sana kuliko zamani.  Hali ya kiwango cha kudhamiria (commitment) kwa wanandoa ni kidogo sana na hivyo kushusha uthamani wa ndoa zenyewe.
Sababu hizi zitakuwezesha kuubadili mtazamo ulionao juu ya ndoa na kukupelekea kubadili namna  unavyo sema au kuwaza au kutenda kuhusiana na suala zima la ndoa.

SABABU MBOVU
  1. Kuingia katika ndoa kwa lengo la kusaidiwa au kuongeza  kiwango cha kiuchumi ulicho nacho.  
hapa wengine wamewageuza wapenzi wao kuwa mitaji au rasilimali ya kuwaondoa wao pamoja na ndugu zao kutoka kwenye umasikini.  Kwa kuthibitisha hili wengine  wamepewa majina kama BUZI, ATM n.k.

Katika penzi la namna hii hakuna mguso au muunganiko wa kuhisia baina ya wapenzi, bali kinachowaunganisha pekee ni kile kilicho mfukoni. Athari za penzi la aina hii lina fungua milango mingi kwa wanandoa  kutokuwa  waaminifu na hata kujihusisha na mapenzi  nje ya ndoa.

  1. Hofu ya umri kupita na kuzeeka
Wako wengi sana, hususani watu wa wajinsia ya kike ambao wamejikuta wakiwakubali wanaume wa aina yoyote ili mradi tu nao waolewe maana umri wao ulionekana kusonga sana na hofu ya kutoolewa kutanda.
Mwanaume anayehusiana na mwanamke mwenye tabia hii huulizwa au kulazimishwa kila siku kwenda kujitambulisha kwa wazazi wa binti au kutangaza ndoa.  Ndoa nyingi za aina hii zimeishia kenye talaka na kutengana.
Wako wengine ambao, kwasababu wanakiu sana ya kupata watoto na wameogopeshwa sana habari kwamba wana weza wasipate watoto kwa sababu ya umri wao, basi watacheka  na kaka yeyote yule ilimradi tu waolewe au wazae naye  Wengine wajinsi hii wamejuta sana baada ya kujikuta kuwa waliyezaa naye hakuwa BABA wa kweli bali kirukanjia tu na kwahiyo wameishia kulea mtoto au watoto wao wenyewe pasipo mzazi wa pili, jambo ambalo kwa kiasi kikubwa  linawaathiri watoto wengi.  Kwa wale wanaokimbilia kuolewa ili wakazae watoto, kukumbuka kuwa hata huko kwenye ndoa kuna waliokosa watoto.

  1. Kuingia kwenye ndoa sababu ya mimba au mtoto aliyepatikana kabla ndoa
Lazima kutofautisha kuwa sababu iliyowapelekea kuzaa mtoto siyo itakayowapelekea kuoana.  Acha sababu ya kuoana kwenu iwe penzi lenu la dhati na sio mimba au mtoto.

Suala hili linahitaji pia wazazi wajue kwamba kitendo cha watoto  kupeana mimba au kupata mtoto hakitoshi kuwa sababu ya kuwalazimisha kuoana, maranyingi wazazi wamewalazimisha watoto wao kuingia katika ndoa sababu ya mimba au mtoto na kujikuta wanawaharibia maisha yao mazima.  

  1. Kulazimika kuingia kwenye ndoa au mahusiano ya kudumu kwasababu ya upweke, (Loneliness). Mara nyingi mtu anapokuwa peke yake (single) huwaza kuwa ndoa ndiyo inayoweza kuwa utatuzi mkubwa wa matatizo yake.  Nakubaliana na ukweli wa maandiko kwamba “Sio vema mtu awe peke yake…” lakini ni vizuri tukijua tofauti iliyopo baina ya kuwa peke yako na upweke.  Hivi ni vitu tofauti: kuwa peke yako inamaanisha kukosa mawasiliano au ukaribu na watu wengine, unakuwa kama uliyetengwa, wakati upweke (loneliness) inahusisha nafsi,  akili na hisia kuwa pweke au kujihisi kutengwa na hii ni ngumu kuishuhulikia.  Ni heri kuwa peke yako (single) kuliko kuwa  kwenye ndoa na bado ukajisikia upweke (lonely).  Wako wengine waliodhani ndoa ni suluhisho la upweke waliokuwa nao na mara walipoolewa au kuoa, mawasiliano baina yao yakayumba na hivyo kukomaza  upweke kwa wote wawili.
  1. Kuolewa au kuoa kwasababu ya shinikizo kutoka kwa wazazi,ndugu au marafiki
Shinikizo hizi zaweza kuwa za kihisia au hata kihalisia.  Kihisia ni pale ndugu au wazazi wanapokushawishi mara kwa mara kuoa sababu umri wako una pita na wako wazazi wengine husema wanataka wajukuu.  Hata kama huhisi  kulazimishwa lakini kwa kule kurudia rudia kwa kukumbushwa kila siku kunaathiri hisia zako na kuweza kukupelekea kuingia katika ndoa isiyopangiliwa.  Shinikizo ya kimwili au kihalisia ni pale wazazi wanopolazimisha watoto wao kuoa au kuolewa na watu fulani kwa sababu tu ni marafiki zao (family friends) au kwa sababu ya kulinda utajiri na matarajio yoyote binafsi.  Ndoa nyingi za aina hii zimekuwa kero na dimbwi la maumivu na machozi, baada ya muda kidogo mna jikuta mali mnazo, wazazi wenu wanapatana,  lakini nyie kama wapenzi ni maadui wakubwa.

  1. Kuamua kuoa au kuolewa ili kupata Uhuru.
Hii hutokea sana kwa wale waliozoea kubanwa sana na wazazi katika kila wafanyacho hususani katika maamuzi.  Wengine huzikimbia familia zao maana hazieleweki, hazina mpangilio na hivyo kutamani kutoka ili wakaanzishe zakwao wenyewe. Kinadada na kinakaka wanachoka kuamuliwa na kuwekewa masharti ya kuvaa, kula, kufanya mambo, kutoka na kurudi kwa muda kwahiyo wanadhani ndoa ndio itawachomoa kifungoni hapo.

MATOKEO YA KUINGIA KATIKA NDOA KWA SABABU MBOVU
Lengo la kuingia kwenye ndoa, liwe zuri au liwe baya ndilo litakalotegemeza aina ya maisha yenu katika ndoa hiyo kuwa ya furaha au ya machungu.  Baada tu ya kuoana na huyo mtu wako kwa sababu zisizo za msingi, siku, miezi au miaka siyo mingi utaanza kuchoka na kutamani kutoka nje ya hiyo ndoa kwamaana baina yenu hakuna muunganiko wa kindani ya ndoa ya jinsi hii.  Na mara nyingi hali hii hupelekea msongo wa mawazo, mfadhaiko na kukosa furaha ndani ya ndoa.  Na matokeo ya hali hii kumfanya mwanandoa mmoja au wote wawili kuanza kutafuta kutoshelezwa na kuliwazwa nje ya ndoa na hapa vinazaliwa vitu kama uzinzi, kutengana na talaka.

Kwanini Ndoa nyingi hushindwa:
Kwa sababu ya kukosa maarifa. Wanandoa wengi hawajui nini wafanye, nini  waelewe ili kufanya ndoa yao zifanikiwe.  Thamani ya ndoa na jinsi ndoa  inavyochukuliwa sikuhizi ni tofauti sana na nyakati za wazazi wetu, na hii imewafanya wengine kujikuta wako wenye ndoa kwasababu mbovu na hivyo ndoa nyingi kuvunjika au kuyumba baada ya muda mfupi tu. Vitu kama kudhamiria, heshima na uaminifu sio vya maana tena siku hizi, sababu watu wanaogopa kuonekana wazamani na washamba. 

Mtazamo wa ulimengu juu ya ndoa umeharibiwa na magazeti, luninga na vitabu mbali mbali.  Siku hizi kuishi bila ndoa ni kitu cha kawaida, kuwa na mpenzi nje ya ndoa sio kitu cha kutisha tena,  mapenzi nje ya ndoa sio ya kushangaza hata kidogo.  Kinyume chake ukionekana kuyashangaa haya, jamii itakushangaa wewe kwa jinsi ulivyo nyuma ya wakati.  Mambo yamebadilika sana, zamani binti akikutwa bikira wakati anaolewa ilikuwa sifa kwake na familia nzima, siku hizi binti akikutwa bikira atachekwa, na watu kumshangaa wakihisi ana matatizo fulani. Hali kadhalika kwa kijana wa kiume aliyejitunza. Kwa bahati mbaya sana  tunaishi katika jamii ya ajabu isiyoamini katika kujitoa kwa kweli na kudhamiria katika ndoa. Jamii isiyoamini katika uaminifu, na ndiyo maana magomvi mengi hutokea pale simu ya mmoja inapoguswa.  Kuwindana na kuchunguzana kumekuwa kawaida, maadili sio jambo la kuzingatiwa tena.  Wanandoa wengi ni wale wenye majeraha ya moyoni na walio umizwa, kwa hiyo hutoka nje ya ndoa zao wakitafutatafuta mwingine aliyeumizwa kama wao ili  waliwazane.

Kwa haraka tuangalie sababu za msingi zinazoweza kukufanya uingie katika ndoa na usijute.
-          Ndoa ni mpango wa Mungu kwa mwanamke na mwanaume kuwa pamoja
-          Ni nafasi ya wawili hawa kuonyeshana mapenzi  yao
-          Ni nafasi ya kutimiziana mahitaji ya mwili kupitia tendo la ndoa kwa muda sahihi, na kwa mtu sahihi, maadili yakizigatiwa.
-          Hamu na kiu ya kutengeneza famila yenu.
-          Kutimiza kiu ya kuwa pamoja kwa umoja (companionship)
-          Nia au kusudi la kushiriki vyote kwa pamoja . Kufanya kutenda kwa pamoja ili kutimiza mahitaji yetu wote.
       -    Nafasi ya kutumia kwa manufaa kila uwezo na vipawa mlivyokuwa    
     navyo.
-          Kuchangiana katika makuzi yenu ya ujumla, makuzi ya kimwili, kiriho, kihisia n.k
 
Na: Chris Mauki
Counselor and Social Psychologist
University of Dar es Salaam
0777 407182, chriss@udsm.ac.tz

No comments:

Post a Comment